WELCOME HMC

2 / 3
3 / 3
3 / 3
2 / 3
Caption Two
3 / 3
Caption Three

Wednesday, 12 April 2017

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora watoa tamko kulaani watu kutekwa

Jana  Jumanne Aprili 11, 2017 Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga ametoa tamko lililoambatishwa kwa vyombo vya habari kuhusiana na matukio ya watu kutekwa na kupotea.
Soma hapa tamko hilo la Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga :
Katika siku za karibuni kumekuwepo  na taarifa katika vyombo vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii, kuhusu matukio ya kupotea au kutekwa kwa wananchi katika mazingira yenye utatanishi, suala ambalo limeibua mijadala katika jamii.
Siku ya Jumatano tarehe 5 Aprili, 2017 msanii wa muziki wa kizazi kipya, Bw. Ibrahim Mussa a.k.a Roma Mkatoliki na wenzake watatu walitekwa wakati wakiwa katika studio za Tongwe Records, eneo la Masaki jijini Dar es Salaam, baada ya kuvamiwa na kundi la watu wasiojulikana. Tarehe 10 Aprili 2017 Bw. Ibrahim Mussa alieleza mbele ya vyombo vya habari jinsi walivyotekwa na kuteswa.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vitendo hivyo, kwani vinaashiria kuwepo kwa makundi yanayoendesha matendo ya utekaji watu kinyume cha sheria.
Matukio ya hivi karibuni ya kuvamia kampuni za tasnia ya habari na mawasiliano au kuwateka watu, yanaashiria kutoweka kwa uvumilivu wa uwepo wa maoni tofauti katika jamii kuhusu mambo mbalimbali.
Kuna matukio yaliyowahi kutokea huko nyuma, kwa mfano, mwandishi wa habari wa Mwananchi Communication Ltd. (MCL) na Deutsche Welle (DW), Bi. Salma Saidi, tarehe 19, Machi 2016, alitekwa na watu wasiojulikana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu  Julius Nyerere, akitokea Zanzibar, na inasemekana aliteswa na kuachiwa baada ya siku kadhaa.  
Pia kumekuwepo taarifa za kutekwa Mkuu wa Idara ya Utafiti na Sera wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Bernard Focus Saanane a.k.a Ben Saanane, aliyetoweka nyumbani kwake eneo la Tabata jijini Dar es Salaam Novemba 18, 2016 na mpaka sasa hajulikani alipo.
Wakati Bi. Salma Saidi na Bw. Ibrahim Mussa na wenzake watatu walionekana baada ya muda mfupi, Bw. Ben Saanane bado hajulikani alipo, yapata miezi mitano sasa.
Uchambuzi wa Tume unaonyesha kuwa waliotekwa wamefanyiwa hivyo kutokana na tasnia yao, au kutumia haki yao ya msingi ya uhuru wa maoni na kujieleza, haki ambazo zimeainishwa na kulindwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (1966), na Ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (1986).
Tanzania ni nchi ambayo imeridhia na kuafiki mikataba hiyo, na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayosisitiza haki hizo. Haki ya kujieleza inaweza kuhojiwa iwapo tu itatumika kinyume na hadhi ya mtu mwingine, au  maslahi ya taifa, kiusalama, kiafya au kimaudhui, na itahojiwa kwa taratibu za kisheria zinazokubalika katika jamii inayoheshimu demokrasia, kwa kuzingatia Katiba ya nchi na mikataba ya Kimataifa.
Tume inapenda kusisitiza kwamba katika nchi yenye demokrasia, serikali ina wajibu na jukumu la kuzilinda haki hizi, na pia kuwalinda wananchi dhidi ya matendo yanayodhalilisha utu wao, utesaji, na matendo yote yanayowanyima uhuru na haki zao za msingi, ikiwemo haki ya maoni na uhuru wa kujieleza.
Kujirudia kwa matukio ya kutekwa watu bila ya serikali kuwakamata wale wanaotekeleza matendo hayo, na kuwapeleka katika vyombo vya sheria, ni jambo la kushangaza, na la aibu kwa taifa. 
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inasikitishwa kuwepo kwa vitendo hivyo katika nchi yetu ambayo imejengeka katika misingi ya haki na demokrasia. Tume inapenda kutoa tahadhari kwamba vitendo kama hivyo na uwepo wa makundi ya kihalifu yanayotekeleza utekaji, utesaji,na mauaji ya watu, yaani (forced disapperance, torture, extra judicial and summary executions) hutokea katika nchi ambazo zinaashiria kuvunjika kwa utawala wa sheria. Vitendo hivi havitakiwi kuvumiliwa kabisa, na Tume haipendi kuamini kwamba nchi yetu inaelekea huko.  
Hivyo basi, Tume inashauri mambo yafuatayo:
  1. Vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, vifanye uchunguzi wa kina kuhusiana na matukio hayo, na kuchukua hatua zipasazo za kisheria kuhakikisha kwamba waliohusika na kupotea kwa Bw. Bernard Saanane, na utekaji wa Bi. Salma Saidi, Bw. Ibrahim Mussa na wenzake wanapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.
  1. Tume inapenda kuvitaka vyombo vya dola vya ulinzi na usalama, kuwahakikishia wananchi kwamba, watu wahusikao na matukio haya siyo watu walioko miongoni mwa vyombo hivyo vya ulinzi na usalama.
  1. Ili kuhakikisha hilo ni vema Jeshi la Polisi likatangaza mapema hatua lilizochukua juu ya mtu aliyeonekana na silaha akimtishia Mhe. Nape Nnauye. Kutosikika kwa hatua zilizochukuliwa kuhusu mtu huyo kunazidi kuacha hisia katika jamii kwamba analindwa asichukuliwe hatua za kisheria.
  1. Tume inawaasa wananchi washirikiane na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa Bw. Bernard Saanane, na zitakazofanikisha kuwapata watekaji wa Bi. Salma Saidi, Bw. Ibrahim Mussa na wenzake.
  1. Mwisho kabisa Tume inapenda kuwakumbusha wananchi wote na vyombo vyote vya serikali, umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria iwapo kuna malalamiko yoyote kuhusu matumizi mabaya ya uhuru wa maoni na haki ya kujieleza, na siyo kuendekeza utekaji na utesaji wa watu, kwani kufanya hivyo ni kujichukulia sheria mkononi na ni ukiukwaji wa sheria, ni matendo yanayotishia amani, na ni kinyume cha haki za binadamu na utawala bora nchini

No comments:

Post a Comment