WELCOME HMC

2 / 3
3 / 3
3 / 3
2 / 3
Caption Two
3 / 3
Caption Three

Tuesday 16 February 2016

NI MSIMU MWINGINE KUTUPELEKA KATIKA KUPATA KATIBA MPYA

Na: Elia Simon Gumbo

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba mpya umeanza baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
 
Kauli hiyo ya Jaji Lubuva imekuja wakati wadau wa siasa nchini wakimtaka Rais Dk. John Magufuli, kutoendelea na Kura ya maoni badala yake mchakato wa Katiba mpya urudi nyuma baadhi ya mambo yaliyo kwenye Katiba iliyopendekezwa yarekebishwe.
 
  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva .
Itakumbukwa kuwa mchakato wa Katiba mpya uliingia dosari baada ya baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga mfumo wa Serikali Tatu uliokuwa umependekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, iliyokusanya maoni nchi nzima na matokeo yake kuzaa kundi lililojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
 
“Tulikuwa tunangoja tumalize uchaguzi, kama vile ambavyo Mnyamwezi anavyobeba mzigo, unamaliza mmoja unakwenda kwa mwingine. Sasa tumemaliza (uchaguzi mkuu), tunakwenda kwa lingine (Kura ya Maoni),” alisema Jaji Lubuva.
 
Aliongeza: “Tunaliangalia na kama Tume tutakuja kuwajulisha wananchi hali ikoje, tuliahirisha (Kura ya Maoni) ili tumalize hili (uchaguzi mkuu).” alisema Jaji Lubuva na kuongeza.
 
“Hili ni suala linalohitaji mambo ya bajeti kubwa na ndiyo tumetoka kwenye uchaguzi na serikali ndiyo inaanza, kwa hiyo ni suala ambalo tunaliangalia na baadaye wananchi watajulishwa,” alisema Jaji mstaafu Lubuva.
 
Alipoulizwa kuhusu makadirio ya bajeti ya kuendesha kura hiyo ya maoni, Lubuva alisema: “Hilo niulize siku nyingine, sina zaidi ya hapo kwa leo.”
 
Rais Magufuli alipokuwa akihutubia Bunge la 11 siku ya kulizindua Novemba 20, mwaka jana, alisema serikali yake imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukukamilika katika awamu iliyomtangulia kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa uandikishaji wapiga kura. 
 
“Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba,” alisema Rais Magufuli.  
 
Mbali na muundo wa serikali tatu, baadhi ya mambo ambayo Ukawa walitaka yawe kwenye Katiba mpya ni mamlaka ya Rais kupunguzwa, ushindi wa Rais uwe zaidi ya asilimia 50, Tume huru ya Uchaguzi, matokeo ya Rais kupingwa mahakamani, kuwe na mgombea binafsi, mawaziri wasitokane na wabunge, na muundo mpya wa Bunge la Muungano.
 
Oktoba 2, 2014, Bunge Maalum la Katiba chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Samuel Sitta, lilipitisha Katiba inayopendekezwa na kuiwasilisha kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Oktoba 8, ili mchakato wa Kura ya Maoni uendelee.
 
Kutokana na kutoka Bungeni kwa wajumbe wa bunge hilo kutoka kundi la Ukawa, kulikuwa na hofu kwamba akidi haitotimia na hivyo Katiba haitapita.
 
Baada ya kura kupigwa, aliyekuwa Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk. Thomas Kashililah, alisema idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum kutoka Zanzibar wakiwamo wa Ukawa waliosusa ambao kura zao zilihesabiwa kuwa ni `Hapana'  jumla yao ni 219.
 
Kwa mujibu wa idadi hiyo, theluthi mbili ya kura hizo kutoka Zanzibar ambazo ndiyo zilizokuwa zikihofiwa zaidi kufanya uamuzi, zilipaswa kuwa 146.
 
Akitangaza matokeo hayo, Dk. Kashililah alisema katika kura za wazi kutoka Zanzibar katika kila ibara, kura za juu kwa ibara moja zilikuwa 109 huku kura za chini zikiwa 106, ambazo hazikutosha kutimiza masharti ya theluthi mbili.
 
Kura za wazi za `Hapana' kwa mujibu wa Dk. Kashililah, kura za juu zilizokataa ni nane huku za chini kukataa ibara za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, zikiwa kura tano.
 
Katika mchanganuo wa kura hizo, kura za siri ndizo zilizookoa jahazi, ambapo ibara iliyopigiwa kura chache zaidi za siri za `Ndiyo' ilipata kura 38 na ibara zilizopata kura za juu zilipata kura 39.
 
Kura za siri za `Hapana' zikiwa kura moja moja na katika ibara chache mno. Baada ya kutangaza matokeo ya kura hizo za wazi na za siri kwa upande wa `Hapana' na `Ndiyo,' ibara zote za Rasimu ya Katiba zilipata kura za chini za 146 na kadirio la juu la kura 148 na kuibua shangwe kubwa, kabla hata ya kura kutoka Tanzania Bara kutangazwa.
 
Kwa upande wa Tanzania Bara kulikuwa na wajumbe  411 wakiwamo wa Ukawa, wajumbe 335 walipiga kura. 
 
Kwa mujibu wa Dk. Kashililah, kila ibara ilipata wastani wa kura 331 mpaka 334, na hivyo kuzidi theluthi mbili iliyokuwa ikihitajika ya 274.

No comments:

Post a Comment