Na Renalda Mwarabu
Makumi ya watu waliokuwa wanashikiliwa na wanachama wa kundi la
kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, wamekombolewa nchini Nigeria.
Mateka waliokombolewa kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.
Sani
Othman, Msemaji wa jeshi la Nigeria ameyasema hayo kupitia ripoti
maalumu juu ya mafanikio ya operesheni za jeshi la nchi hiyo na Cameroon
na kuongeza kuwa, askari wa nchi hizo mbili wamefanikiwa kukomboa
mateka 112 kutoka mikononi mwa kundi hilo kupitia operesheni za pamoja.
Othman amesema kuwa, miongoni mwa watu waliokombolewa katika
operesheni hizo zilizofanyika katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki
mwa Nigeria, ni pamoja na wanaume wanane, wanawake 36 na watoto 68.
Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, operesheni za kuwakomboa
watu hao zimezaa matunda kwa ushirikiano wa jeshi la nchi jirani ya
Cameroon katika kupambana na wanachama wa kundi hilo la kigaidi la Boko
Haram.
Ameongeza kuwa, katika operesheni hizo afisa mmoja wa jeshi la
Cameroon amejeruhiwa vibaya baada ya gari alilokuwa ndani yake
kulipukiwa na bomu katika moja ya vijiji vya jimbo hilo la Borno.
Hadi sasa zaidi ya watu elfu 17 wameuawa katika mashambulio ya
wanachama wa genge hilo lililotangaza uungaji wake mkono kwa kundi la
kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Inelezwa kuwa, hadi sasa mamia ya watu
wakiwamo wanafunzi wa kike bado wanashikiliwa na wanachama wa Boko Haram
nchini Nigeria.(Kutoka mtandaoni).
No comments:
Post a Comment