Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba mpya umeanza baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Kauli hiyo ya Jaji Lubuva imekuja wakati wadau wa siasa nchini
wakimtaka Rais Dk. John Magufuli, kutoendelea na Kura ya maoni badala
yake mchakato wa Katiba mpya urudi nyuma baadhi ya mambo yaliyo kwenye
Katiba iliyopendekezwa yarekebishwe.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva . |
Itakumbukwa kuwa mchakato wa Katiba mpya uliingia dosari baada ya
baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga mfumo wa
Serikali Tatu uliokuwa umependekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph
Warioba, iliyokusanya maoni nchi nzima na matokeo yake kuzaa kundi
lililojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Tulikuwa tunangoja tumalize uchaguzi, kama vile ambavyo Mnyamwezi
anavyobeba mzigo, unamaliza mmoja unakwenda kwa mwingine. Sasa
tumemaliza (uchaguzi mkuu), tunakwenda kwa lingine (Kura ya Maoni),”
alisema Jaji Lubuva.
Aliongeza: “Tunaliangalia na kama Tume tutakuja kuwajulisha
wananchi hali ikoje, tuliahirisha (Kura ya Maoni) ili tumalize hili
(uchaguzi mkuu).” alisema Jaji Lubuva na kuongeza.
“Hili ni suala linalohitaji mambo ya bajeti kubwa na ndiyo tumetoka
kwenye uchaguzi na serikali ndiyo inaanza, kwa hiyo ni suala ambalo
tunaliangalia na baadaye wananchi watajulishwa,” alisema Jaji mstaafu
Lubuva.
Alipoulizwa kuhusu makadirio ya bajeti ya kuendesha kura hiyo ya
maoni, Lubuva alisema: “Hilo niulize siku nyingine, sina zaidi ya hapo
kwa leo.”
Rais Magufuli alipokuwa akihutubia Bunge la 11 siku ya kulizindua
Novemba 20, mwaka jana, alisema serikali yake imepokea kiporo cha
mchakato wa Katiba ambao haukukamilika katika awamu iliyomtangulia
kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa uandikishaji wapiga kura.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya
kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya
ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na
Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza
wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba,”
alisema Rais Magufuli.
Mbali na muundo wa serikali tatu, baadhi ya mambo ambayo Ukawa
walitaka yawe kwenye Katiba mpya ni mamlaka ya Rais kupunguzwa, ushindi
wa Rais uwe zaidi ya asilimia 50, Tume huru ya Uchaguzi, matokeo ya Rais
kupingwa mahakamani, kuwe na mgombea binafsi, mawaziri wasitokane na
wabunge, na muundo mpya wa Bunge la Muungano.
Oktoba 2, 2014, Bunge Maalum la Katiba chini ya aliyekuwa
Mwenyekiti wake, Samuel Sitta, lilipitisha Katiba inayopendekezwa na
kuiwasilisha kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Oktoba 8,
ili mchakato wa Kura ya Maoni uendelee.
Kutokana na kutoka Bungeni kwa wajumbe wa bunge hilo kutoka kundi
la Ukawa, kulikuwa na hofu kwamba akidi haitotimia na hivyo Katiba
haitapita.
Baada ya kura kupigwa, aliyekuwa Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk.
Thomas Kashililah, alisema idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum kutoka
Zanzibar wakiwamo wa Ukawa waliosusa ambao kura zao zilihesabiwa kuwa ni
`Hapana' jumla yao ni 219.
Kwa mujibu wa idadi hiyo, theluthi mbili ya kura hizo kutoka
Zanzibar ambazo ndiyo zilizokuwa zikihofiwa zaidi kufanya uamuzi,
zilipaswa kuwa 146.
Akitangaza matokeo hayo, Dk. Kashililah alisema katika kura za wazi
kutoka Zanzibar katika kila ibara, kura za juu kwa ibara moja zilikuwa
109 huku kura za chini zikiwa 106, ambazo hazikutosha kutimiza masharti
ya theluthi mbili.
Kura za wazi za `Hapana' kwa mujibu wa Dk. Kashililah, kura za juu
zilizokataa ni nane huku za chini kukataa ibara za Rasimu ya Katiba
Inayopendekezwa, zikiwa kura tano.
Katika mchanganuo wa kura hizo, kura za siri ndizo zilizookoa
jahazi, ambapo ibara iliyopigiwa kura chache zaidi za siri za `Ndiyo'
ilipata kura 38 na ibara zilizopata kura za juu zilipata kura 39.
Kura za siri za `Hapana' zikiwa kura moja moja na katika ibara
chache mno. Baada ya kutangaza matokeo ya kura hizo za wazi na za siri
kwa upande wa `Hapana' na `Ndiyo,' ibara zote za Rasimu ya Katiba
zilipata kura za chini za 146 na kadirio la juu la kura 148 na kuibua
shangwe kubwa, kabla hata ya kura kutoka Tanzania Bara kutangazwa.
Kwa upande wa Tanzania Bara kulikuwa na wajumbe 411 wakiwamo wa Ukawa, wajumbe 335 walipiga kura.
Kwa mujibu wa Dk. Kashililah, kila ibara ilipata wastani wa kura
331 mpaka 334, na hivyo kuzidi theluthi mbili iliyokuwa ikihitajika ya
274.
No comments:
Post a Comment