WAKATI Spika wa Bunge, Job Ndugai akiipiga ‘kijembe’ Yanga kwa kupoteana ndani na nje ya uwanja huko Algeria, benchi la ufundi la klabu hiyo limesema “tumesahau” yaliyotokea na kwamba nguvu na akili zao sasa wamezielekeza katika mechi ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA-
dhidi ya Tanzania Prisons itakayopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo ni ya kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi wakati akizungumza na Nipashe jana, ambaye pia aliweka wazi kuwa kuondolewa kwenye michuano ya kimataifa hakujamaliza nguvu za wachezaji wao katika kutetea ubingwa wa Kombe la FA na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga ilikubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya MC Alger ya Algeria na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-1 katika kinyang’anyiro cha kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni baada ya kushinda bao 1-0 kwenye mechi ya awali jijini Dar es Salaam.
Lakini Mwambusi alisema hayo wameyasahau na kwamba ili kujiimarisha, kundi la kwanza la wachezaji wa timu hiyo ambao wameshawasili nchini, jana jioni lilitarajia kuanza mazoezi kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi.
"Kilichotokea Algeria tumeshafunga kurasa zake, kwa sasa hakuna kulala, wachezaji waliopo wanaanza mazoezi leo (jana) na kesho (leo) kikosi kitakapokuwa kimekamilika mazoezi yataendelea kwa kasi, hatuna muda wa kupoteza tena," alisema Mwambusi.
Kocha huyo alisema lengo lao ni kushinda mechi hiyo ya Jumamosi ili waweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayotoa mwakilishi wa nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufanya vizuri mechi zilizobakia za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu za Simba, Azam FC za Dar es Salaam na Mbao FC ya jijini Mwanza, tayari zimeshatinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho.
Baada ya mechi hiyo ya Jumamosi, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wataikaribisha tena Prisons katika mechi ya ligi itakayofanyika Mei 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.
Kijembe cha Ndugai
Katika hatua nyingine Spika Ndugai ameipiga kijembe Yanga kwa kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya MC Alger ya Algeria akidai kuwa kiliwachanganya hadi wakapoteana.
Ndugai alitoa kauli hiyo bungeni jana baada ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura kujibu maswali ya Mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia aliyetaka kujua kuwa serikali imefikia wapi katika suala la hatimiliki ili wasanii, wanamichezo na wanamitindo wetu waweze kupata haki zao.
Katika majibu yake, Wambura aliwaalika wasanii wote pale watakapokuwa wakizungumzia masuala yao kila Jumanne ya kila mwezi kufika ofisini kwake Dar es Salaam na Dodoma.
Baada ya kauli hiyo, Spika alichomekea akisema “tunamuunga mkono Naibu Waziri kuwa tukazanie masuala ya sanaa maana mambo ya mpira wa miguu yanatupa shida kidogo.”
Ndugai aliendelea kueleza: “Watu wamepoteana uwanjani kwa bao nne, wakapoteana mjini, wanarudi mafungu mafungu, namuuliza mheshimiwa Waziri Mkuu vipi, anasema haelewi kinachoendelea
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular Posts
|
|
No comments:
Post a Comment