Mkuu wa Jeshi la polisi nchini (IGP), Simon Sirro amewataka makamanda wa polisi mikoa kuhakikisha wanatumia vizuri mafuta ya magari wanayowekewa ili kuepuka malalamiko ya wananchi kwa magari ya polisi kukosa mafuta.
Pia amesema hataki kusikia polisi hawajafika katika tukio kutokana na kisingizio cha kutokuwa na mafuta.
IGP Sirro alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro na kuongeza kuwa ni kosa kwa mwananchi kudaiwa fedha za mafuta ya gari la polisi.
IGP Sirro yupo katika ziara ya kuangalia hali ya uhalifu katika mikoa akitokea mkoani Dodoma.
Alisema mafuta ya gari yapo katika bajeti ya Jeshi la Polisi kwa kila mkoa hivyo kinachotakiwa ni makamanda wa mikoa kuhakikisha kuwa wanayatumia vizuri.
“Ni jambo la kusikitisha mwananchi kutakiwa kuchangia mafuta ya gari la polisi,hili hatuliruhusu kabisa,” alisema Sirro
Hivi karibuni, wakazi wa Malinyi walimlalamikia Mkuu wa Wilaya hiyo Jacob Kassema kwa kuwachangisha Sh800,000 za mafuta ya gari lake. Hata hivyo, Kassema alikanusha suala hilo.
Mbali ya suala la mafuta, IGP Sirro aliwatoa hofu wananchi na kusema Serikali inaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu mauaji yanayoendelea mkoani Pwani.
“Ni kweli kuna tatizo la mauaji Pwani lakini askari wetu wapo kazini mchana na usiku kutafuta suluhisho la tatizo,” alisema Sirro
No comments:
Post a Comment