ULAYA WAMGOMEA
MAGUFULI
Na Abeli said Lowassa
11th February 2016
Rais Dk. John Magufuli. |
Umoja wa Ulaya (EU), umemgomea Rais Dk. John Magufuli, kwa
kueleza kuwa msimamo wake uliotolewa na washirika wa jumuiya ya kimataifa wa
kumtaka kushirikiana na vyama vilivyoshiriki uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar
kufikia muafaka.
Akijibu swali kutaka
kujua walivyopokea ombi la Rais kwa jumuiya za kimataifa kuzungumza na CUF, ili
wakubali kushiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka
huu, Msemaji wa EU, Balozi Roeland van de Geer, alisema wanasubiri kuona
utekelezaji wa tamko lao.
"Msimamo wa
washirika kadhaa wa jumuiya ya kimataifa nchini, Umoja wa Ulaya na nchi
wanachama wakizungumzia kuhusu uchaguzi wa marudio kufanyika, umeelezewa bayana
kwenye tamko lilitolewa Januari 29, mwaka huu," alisema Balozi Roeland na
kuongeza:
"Mpaka sasa EU hatuna la kuongeza zaidi ya tamko hilo
linaloelezea msimamo wetu kwa ukamili. Hata hivyo, kwa sasa tunaendelea
kufuatilia kwa ukaribu maendeleo yake na tunatumaini maendeleo hayo yataleta
habari njema kwa wote visiwani humo."
Januari 29, mwaka
huu, EU jumuiya ya kimataifa inayojumuisha nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark,
Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania,
Sweden, Uswisi, Marekani na Uingereza
zenye ubalozi nchini, zilitoa tamko la pamoja la kumtaka Rais kuingilia katika
mgogoro huo.
‘’Tunamtaka Rais
Magufuli kuonyesha uongozi wake kupitia mgogoro huu wa kisiasa kwa kuingilia
kati na kutafuta usuluhishi baina ya vyama vikuu kuhakikisha amani pande
zote," ilisema sehemu ya tamko hilo.
Tamko hilo pia
lilieleza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa uchaguzi wa Oktoba 25,
mwaka jana, ulikuwa na kasoro zilizoelezwa na kwamba waangalizi wa kutoka Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika
(AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki, EU, Marekani na Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) waliridhika na mwenendo wa uchaguzi huo.
Walisema wakati
mazungumzo baina ya CUF na CCM yakiendelea, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alitangaza uchaguzi wa marudio.
Tamko hilo lilisisitiza
kurejewa kwa mazunguzo ya vyama vinavyovutana na kuwa na maridhiano kuliko
kurudi kwenye uchaguzi mpya.
Walisema kurudiwa kwa uchaguzi huo kutaongeza hali ya
wasiwasi na sitofahamu visiwani humo, hivyo ni vyema pande zote (CUF na CCM)
zikakutana na kuwa na makubaliano ya pamoja na ya amani.
"Ili uwe
uchaguzi huru na haki ni lazima pande zote zishiriki. Kwa hali iliyopo kwa sasa
itakuwa vigumu kwa waangalizi wa kimataifa kushiriki uchaguzi wa marudio,"
lilifafanua tamko hilo.
Mwanzoni mwa Desemba,
mwaka jana, waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) walitoa wito kwa
ukamilishwaji wa haraka wa mchakato wa uchaguzi Zanzibar kulingana na kanuni za
uchaguzi shirikishi, za uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na kuaminika.
Mwangalizi Mkuu wa EU
EOM, Judith Satgentini, alisema: “EU EOM iko tayari kurejea nchini kuangalia
mchakato wa uchaguzi Zanzibar pindi makubaliano ya kuendelea
yatakapofikiwa."
Jecha alitoa tamko la
kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 25, mwaka jana, baada ya kueleza
kasoro tisa zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo.
Kumekuwa na mvutano
baina ya chama tawala (CCM) na chama kikuu cha upinzani visiwani humo (CUF).
Katika mvutano huo, CUF inataka kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba
25, ambao mgombea urais wake, Maalim Seif Sharif Hamad, alijitangaza mshindi
kwa kupata kura 200,007 dhidi ya 178,363 alizopata mgombea wa CCM, Dk. Ali
Mohammed Shein.
Hivi karibuni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga,
alisema: “Baadhi ya watu, mashirika, EU, Marekani, Jumuiya ya Madola na wote
walioona kwamba tume haikutenda haki (Zec kufuta matokeo ya Uchaguzi wa
Zanzibar)… kwamba ingemaliza kuhesabu na matangazo yatoke. Lakini tume iliona
kabisa kwamba ikifanya hivyo itakuwa imekiuka maadili yake,“ alisema.
“Kwa hiyo kukawa na
mvutano. Kwamba kwa upande wa vyama, walivyopewa maamuzi haya ya tume, wakakaa
kuona wafanye nini. Na tukadhani katika hivi vyama kuzungumza kule, na sisi
bara watatukaribisha, au Serikali ya Muungano watatukaribisha. Lakini wakasema
hata, hili mtuachie sisi wenyewe tutalizungumza kuhusu huu uamuzi wa tume,”
alisema Balozi Mahiga.
“Wengine wakasema
hata misaada tunasimamisha, kama vile Marekani (Fedha za MCC)… tunasimamisha
kwa sababu sisi tunaona haya mazungumzo hayatoi majibu na afadhali tu
yatangazwe (matokeo ya uchaguzi) kama yalivyokuwa, lakini katika hilo baadaye
tume ikasema jamani, afadhali tuite uchaguzi mwingine.
Akijibu baadhi ya
hoja za wabunge zilizotolewa wakati wa mjadala wa Mwongozo wa Kuandaa Mpango na
Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa 2016/17 Bunge,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema Rais Magufuli
hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia masuala ya Zanzibar.
“Kile ambacho baadhi
ya wabunge wamekisema hapa ni kama kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuingilia mamlaka ya Zanzibar na tafsiri yake ni kama unataka kuleta
hoja ya kujenga serikali moja,” alisema Masaju.
“Hoja kwamba Rais
Magufuli aingilie haiwezekani. Mambo ya ulinzi na usalama ndio ya muungano na
hicho ndicho kinafanyika Zanzibar kuhakikisha amani na usalama," alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment