MWANAMKE TARIME
AWANYANG’ANYA MAJAMBAZI BUNDUKI SMG.
Na Abeli Said Lowassa
11th February 2016
Mwanamke wa kitongoji cha Buriba, kata ya Sirari, wilayani
Tarime, anayejishughulisha na biashara ya kuuza kibanda cha duka, Sophia
Manguye (46), amefanikiwa kuwanyang'anya majambazi watatu bunduki moja aina ya
SMG yenye risasi 27, baada ya kupambana nao ndani ya kibanda chake cha
biashara.
Majambazi hao kabla
ya kunyang'anywa bunduki, yalifanya uporaji katika vibanda kadhaa vya maduka na
kufanikiwa kujikusanyia zaidi ya Sh. 180,000, pamoja na vocha za simu za
mkononi kutoka maduka matatu tofauti.
Jambazi aliyeporwa
bunduki hiyo na Sophia ni Gesanta Matinde (19), mkazi wa kijiji cha Kebeyo,
kata ya Mbogi, ikiwa na risasi 27.
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Tarime/Rorya, Gemini Mushi, jana alisema tukio hilo la uvamizi na
unyang'anyi kwa wafanyabiashara lilitokea juzi saa 2:00 usiku katika kitongoji
cha Buriba, mji mdogo wa Sirari, baada ya majambazi watatu waliokuwa na silaha
aina ya SMG namba UK 5115 kuwavamia wafanyabiashara hao.
“Awali majambazi hao
waliingia duka la Zaituni Magasi lililopo jirani na la Sophia na kupora fedha
taslimu Sh. 100,000 kabla ya kuingia dukani kwa Sophia na kupora 80,000 za
mauzo, lakini hawakuridhika na kiasi hicho, hivyo kuingia ndani na kuanza
kutafuta fedha nyingine,” alisema Kamanda Mushi.
Hata hivyo, Kamanda
Mushi alisema wakati wakiendelea kupekua kutafuta fedha nyingine, mwanamke huyo
alimvamia jambazi aliyekuwa na silaha kisha kumng’ang’ania kwa nguvu, huku
akipiga kelele za kuomba msaada hadi walipojitokeza wananchi na polisi
waliokuwa karibu kutoa msaada.
Kamanda Mushi alisema
baada ya tukio hilo, majambazi wawili walifanikiwa kutoroka, huku mwanamke huyo
akipata majeraha usoni na mikononi wakati wa kupambana na majambazi hao.
Alisema Jeshi la
Polisi limempongeza mwanamke huyo kwa ujasiri aliouonyesha pamoja na wananchi
waliojitokeza na kuongeza nguvu na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa na bunduki
hiyo ambayo ingeleta madhara makubwa kwa wananchi.
Aliwaomba wananchi
kushiriki ulinzi shirikishi kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi hilo mapema
kabla ya matukio.
Alisema kwa sasa wanaendelea kumhoji mtuhumiwa na wengine
wawili waliotoroka wakitafutwa ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.
CHANZO: IPP MEDIA
No comments:
Post a Comment